Kituo hiki kilizinduliwa kama sehemu ya mpango wa utafiti unaolenga kufanya tathmini ya ufanisi wa teknolojia za kisasa za ufugaji barani Afrika. Mpango huu umeundwa ili kuimarisha matumizi ya teknolojia bunifu katika ufugaji wa mifugo, lengo kuu likiwa ni kuongeza uzalishaji, ufanisi, na faida kwa wafugaji. Mradi huu unatumia teknolojia za kisasa kama vile sensors, ambavyo vinamwezesha mfugaji kumfuatilia ng’ombe wake kwa ukaribu, kupata taarifa kwa wakati kuhusu afya, mwenendo na uzalishaji , na hivyo kumsaidia kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati.
Technologia hizi zitafanyiwa majaribio kwa wafugaji wadogo wa ng’ombe wa maziwa nchini Tanzania, na lengo ni kuzifanya ziwafikie kwa urahisi, hivyo kuboresha namna wanavyosimamia mifugo yao kwa tija zaidi. Kupitia Kituo hiki, pia tumejikita katika kutoa mafunzo kwa wafugaji juu ya mbinu bora za ufugaji wa kisasa, ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia hizi, lishe bora ya mifugo, pamoja na usimamizi wa afya ya wanyama.
Kama kitovu cha utafiti na mafunzo, wafugaji wana fursa ya kutembelea kituo hiki kwa ajili ya kujifunza kwa njia ya vitendo. Wataweza kuona teknolojia hizi zikifanya kazi moja kwa moja mashambani na kupata elimu ya vitendo kuhusu jinsi ya kuzitumia kwa mafanikio. Zaidi ya hayo, kituo hiki kitakuwa ni sehemu muhimu ya kubadilishana mawazo na uzoefu kati ya wataalamu wa mifugo, wanasayansi, na wafugaji, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa sekta ya mifugo kwa ujumla.
Jiunge nasi katika Kituo chetu, tunapojenga njia kuelekea mustakabali mzuri na endelevu wa sekta ya ufugaji. Hapa, mila bora za ufugaji zinachanganyika na ubunifu wa kiteknolojia za kisasa ili kutoa matokeo ya kipekee kwa wafugaji na jamii kwa ujumla. Tunahakikisha kuwa sekta ya ufugaji inakuwa endelevu, yenye tija, na inayoweza kuhimili changamoto za mazingira na soko la kisasa.