Chuo Kikuu cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia ya Afrika (NM-AIST) kimezindua rasmi Kituo cha Utafiti wa Teknolojia za Kisasa kwa Ufugaji Fanisi (Precision Livestock Farming Hub – PLF Hub)
Kituo hicho kilichozinduliwa Aprili 11,2025 katika Kampasi ya Tengeru jijini Arusha, kinaratibiwa na Mradi wa tathmini ya ufanisi wa teknolojia za kisasa za ufugaji wa mifugo barani Afrika kwa ufadhili wa Bill na Melinda Gates Foundation. Lengo ikiwa ni kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji wa ng’ombe wa maziwa katika kupata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu maradhi, lishe na upandishaji joto kwa wanyama.
Katika hotuba yake ya uzinduzi, Prof. Maulilio Kipanyula ambaye ni makamu mkuu wa chuo, alieleza kuwa moja ya mafanikio ya awali ya kituo hiki ni matumizi ya vifaa maalum vya kidigitali vinavyowekwa ndani ya tumbo la ng’ombe (boluses) ambavyo hutoa taarifa kwa wakati kuhusu mwenendo wa mnyama, taarifa kama; kama ng’ombe anatarajia kuingia joto, anadalili za ugonjwa,, mahitaji ya ng’ombe ikiwemo kiasi cha chakula au maji alichokula au anachohitaji. Taarifa hizi mfugaji anazipata kupitia simu yake, na kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati.
Kwa sasa, jumla ya wafugaji 95 kutoka vijiji vitano vya Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro tayari wameshapokea vifaa hivyo na wameanza kupata manufaa ya moja kwa moja. Aidha, mpango wa kutoa mafunzo kwa wafugaji wengi zaidi uko mbioni kutekelezwa ili kuhakikisha teknolojia hii inaenea kwa upana zaidi, ikilenga kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa na kuboresha maisha ya wafugaji vijijini.
Kwa kutumia teknolojia hii, wafugaji hawatalazimika tena kutegemea dalili za macho au uzoefu pekee kutambua kama ng’ombe anaumwa au yuko tayari kupandwa. Sasa, kila taarifa muhimu inapatikana moja kwa moja kupitia mfumo wa kidigitali.
Kituo hiki pia kimepangwa kuwa kitovu cha mafunzo, tafiti na ubunifu kwa watafiti, wanafunzi, watendaji wa serikali na sekta binafsi, kwa lengo la kukuza matumizi ya teknolojia katika mifumo ya ufugaji. Vifaa vinavyotumika vinajumuisha boluses za ndani ya mwili, na hereni za masikioni, pamoja na mfumo wa kuchambua taarifa ili kusaidia kutoa mapendekezo ya kitaalamu kwa wafugaji.
PLF Hub inatarajiwa kuwa mfano wa kuigwa Tanzania na barani Afrika, kwa kuwa inachanganya utafiti wa hali ya juu na matumizi ya moja kwa moja kwa jamii, kwa njia jumuishi inayowaleta pamoja watafiti, wafugaji, na watunga sera.